Wenger ndiye meneja aliyeshinda vikombe vingi zaidi vya FA |
Meneja wa Arsenal Arsene Wenger anaamini klabu hiyo iliwajibu wakosoaji kwa uchezaji "imara na wa pamoja" walipowalaza Manchester City na kufika fainali ya Kombe la FA kwa mara ya kwanza katika miaka minne.
Alexis Sanchez alifunga bao muda wa zaida na kusaidia Gunners kutoka nyuma na kushinda 2-1.
Hii itakuwa mara ya 20 kwa Arsenal kufika fainali, na mara ya nane chini ya Wenger.
"Mnaweza kutengana au kuwa na umoja na tulitoa jibu sahihi."
Wenger, 67, amekabiliwa na ukosoaji na upinzani mkali zaidi msimu huu, ambao ni wake wa 21 kwenye hatamu Arsenal, kutokana na kutofana kwa klabu hiyo.
Arsenal kwa sasa wamo nafasi ya saba Ligi ya Premia.
Walilazwa jumla ya 10-2 na Bayern Munich katika Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.
Mkataba wa Wenger katika klabu hiyo unamalizika mwisho wa msimu. Amepewa mkataba mpya wa miaka miwili lakini bado hajatangaza uamuzi wake.
baadhi ya mashabiki wa Arsenal wamekuwa wakiandamana dhidi ya meneja huyo miezi ya karibuni.
"Ninahisi kwamba klabu hii imo katika hali nzuri, na kwamba kwa jumla tuna kikosi imara," alisema.
"Siku moja bila shaka nitaondoka, lakini la muhimu ni kwamba Arsenal itasalia kuwa klabu kubwa ambayo inaenziwa na kila mtu.
"Ulikuwa mtihani mgumu sana kweli, mtihani wa kiakili kwa sababu watu wengi hutilia shaka uwezo wetu kufanya nyakati kama hizi.
"Ilikuwa mechi ngumu lakini kwa jumla tulistahili kushinda. Wachezaji walionesha umoja."
Wenger pia alisema anatarajia mshambuliaji wa zamani Barcelona aendelee kusalia Emirates.
Alisema: "Alexis Sanchez kwa sasa ni kama timu. Alikuwa na matatizo mwanzoni lakini akaimarika na kuimarika.
"Yeye ni mnyama, aliye tayari kuua mpinzani. Huwa hakati tamaa.
"Atakuwepo hapa mwaka ujao kwa sababu ana mkataba na twatumai tutafanikiwa kuongeza mkataba wake."
No comments:
Post a Comment