Serikali ya Korea Kaskazini imetoa tamko la msimamo mkali kufuatia hatua ya Marekani
kusogeza meli zake za kivita katika rasi ya nchi hiyo siku chache zilizopita.
Nchi hiyo imetangaza kuwa inaendelea na mpango wake wa kufanya jaribio kubwa zaidi la bomu na makombora ya nyuklia litakalokuwa la sita na kwamba hawatakoma hata kama Marekani itaendelea na mipango yake ambayo wamedai ni ya chuki.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Haki za Binadamu kwenye Chuo cha Jamii cha Korea Kaskazini aliyepewa mamlaka ya kuzungumzia masuala ya mgogoro wa nchi hizo mbili, Sok Chol Won jana aliiambia CNN kuwa mpango huo kabambe uko palepale.
“Majaribio ya mabomu na makombora ya nyuklia ni muhimu kwetu kama sehemu ya juhudi za kuimarisha nguvu zetu za nyuklia,” alisema.
“Wakati ambapo Marekani inaendelea na hatua zake za chuki na hasira, majaribio ya nyuklia na makombora hayatakoma,” alisisitiza.
Kauli hiyo imekuja wakati ambapo Baraza la Mawaziri la Marekani limeweka msisitizo wa kuiwekea Korea Kaskazini vikwazo vya kiuchumi na kidiplomasia huku ikitoa wito pia wa kuwepo kwa mazungumzo.
Hata hivyo, Rais Donald Trump na Makamu wake wamesisitiza uwezekano wa kuwepo hatua za kijeshi dhidi ya Korea Kaskazini.
No comments:
Post a Comment