Labels

Wednesday 26 October 2016

Justin Timberlake nusura ajipate taabani kwa sababu ya selfie

Justin Timberlake

Mwanamuziki mashuhuri nchini Marekani Justin Timberlake nusura ajipate taabani  baada yake kupakia picha yake ya kujipiga kwenye mtandao wa Instagram.
Alikuwa amejipiga picha hiyo akipiga kura yake katika mji wa Memphis, Tennessee.
Yeye ni miongoni mwa mamilioni ya wapiga kura ambao wamekuwa wakipiga kura zao mapema.
Nyota huyo wa pop, ambaye pia ni mwigizaji, hakuwa anakumbuka kwamba jimbo la Tennessee lilipiga marufuku upigaji wa picha katika vitu vya kupigia kura mwaka jana.
Afisi ya mwanasheria mkuu wa eneo la Shelby ilikuwa awali imesema "imefahamishwa kuhusu uwezekano wa uvunjaji wa sheria za uchaguzi" na kwamba kisa hicho kilikuwa kinachunguzwa.
Lakini baadaye, mwanasheria huyo Amy Weirich alisema taarifa hiyo ya awali "haikuwa sahihi" na lilitolewa kwa umma bila yeye kufahamu.
"Niko nje ya mji kwa sasa nikihudhuria kongamano. Hakuna yeyote katika afisi yetu anayechunguza kisa hiki kwa sasa. Hatutatumia rasilimali zetu adimu kufuatilia suala hili," alisema Bi Weirich.
Timberlake ana wafuasi 37 milioni kwenye Instagram.
Iwapo angefunguliwa mashtaka ya kukiuka sheria za uchaguzi, angehukumiwa kufungwa jela siku 30 au kupigwa faini $50 (£41), au apewe adhabu zote mbili.
Adam Ghassemi, msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Tennessee, amesema watu wanafaa kutumia simu zao kujisaidia katika kupiga kura pekee.


Justin Timberlake

Ni kinyume cha sheria kupiga picha katika chumba cha kupigia kura katika majimbo 18 nchini Marekani kwa mujibu wa shirika la habari la AP.
Hata hivyo, katika majimbo 20 inakubaliwa.
Jumatatu, jaji mmoja wa mahakama ya dola aliunga mkono msimamo wa mwanamume mmoja kutoka Michigan kwamba sheria inayowazuia watu kupiga picha kura zao ambazo tayari wamezijaza na kuzisambaza picha hizo mitandaoni ni ukiukaji wa haki ya kikatiba ya kujieleza.
Jumatatu, wapiga kura wengine wawili jimbo la Colorado waliwasilisha kesi kortini kupinga sheria inayozuia watu kuonyesha karatasi za kura ambazo wamezijaza kwa watu wengine. Wanasema marufuku hiyo inakiuka katiba.

No comments:

Post a Comment