Labels

Tuesday 25 April 2017

Simba yaamua kukaa kimya

Uongozi wa Klabu ya Simba umesema hauwezi kuzungumzia kitendo cha wao kupokonywa pointi tatu na Kamati ya Sheria, katiba na Hadhi za wachezaji mpaka hapo watakapopewa nakala ya maamuzi ya kikao cha kamati hiyo.
Makamu wa Rais wa Simba, Godfrey Nyange (Kaburu) alisema wamesikia taarifa kupitia mitandao na vyombo mbalimbali vya habari kuwa wamepokwa pointi walizopewa na Kamati hiyo.
''Habari hizo zilizotolewa na viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambazo zinaonesha kutokuzingatia kanuni na taratibu katika kupokonya pointi zetu kiukweli zina mapungufu makubwa''.alisema Kaburu
Aidha Kaburu, alisema kuwa wanashangazwa na kitendo cha katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, Selestine Mwesigwa kukiri kuwa Mchezaji wa Kagera Sugar Fakh Mohammed, alikuwa na kadi tatu hivyo kuamua kuinyang'anya Simba pointi kutokana na kutotimiza baadhi ya vigezo wakati wa kudai haki yao.
Alisema wanashangaa kuona TFF inashindwa kutimiza majukumu yao wenyewe pasipo kusubiri klabu ziende kupeleka malalamiko na ndipo waweze kuchukua maamuzi wanayopaswa kuyachukua.
"Hili suala lipo wazi kutokana na wao wenyewe kukiri kwamba Faki, alikuwa ana kadi tatu pasipo kujali kama sisi tumekata rufaa au hatujakata, pia hatujajua ni mambo gani yanayoendelea kwa sababu mpaka hivi sasa hatujapata barua rasmi inayotueleza kile kilichofanyika kwa siku zote ambazo kamati ya Sheria, Katiba na Hadhi za wachezaji walijadili kwa siku zote," alisema Kaburu.
Wakati huo huo, Katibu mkuu wa Yanga, Boniface Mkwasa aliitaka TFF ku badili kanuni na taratibu zinazoruhusu timu Fulani kupewa pointi za mezani endapo wanakuwa wameshindwa kupata ushindi katika Michezo yao ya awali.
Alisema kitendo cha kutoa pointi za mezani kinazidi kuzorotesha soka la Tanzania na timu ndogo ndogo zimekuwa ndio waathirika wakubwa wa vitendo hivyo.






No comments:

Post a Comment